John Mapepele Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameipongeza Kampuni ya Wasafi kwa kukuza sanaa ya muziki na kuzalisha ajira kwa vijana wengi hapa nchini. Akizungumza kwenye hafla ya Usiku wa Mahaba Ndi Ndi Ndi siku ya wapendanao Februari 14, 2022 jijini Dar es Salaam amesema Wasafi ina mchango mkubwa katika kuibua na kukuza vipaji vya wanamuziki. " Naomba nikuhakikishie Serikali ipo pamoja na nyie katika kukuza sanaa " amesema Mhe.Mchengerwa Aidha, amesema Serikali inakwenda kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wasafi mtaa kwa mtaa, kijiji kwa kijiji hadi mkoa kwa mkoa kutafuta vipaji vya wasanii lengo ni kuwashindanisha na kuwaendeleza. Ameongeza kuwa, wizara inakwenda kuendeleza mapinduzi ya ukuzaji wa Sanaa ili kutoa ajira zaidi kwa vijana katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Amefafanua kwamba kufanya hivyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kutaka kuboresha sekta hiyo ili wasanii nchini waweze kunufaika na kazi zao. Kwa upande mwingine Mhe. Mchengerwa amesema, katika kipindi hiki sanaa inakwenda kutumika kuitangaza Tanzania kimataifa. Naye Mtendaji Mkuu wa Wasafi, Msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya barani Afrika, Diamond Platinum ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga mazingira wezeshi kwenye Sekta ya Sanaa nchini. Waziri Mchengerwa akitoa salamu za Serikali kwenye usiku wa Mahaba ndi ndi ndi Mtendaji Mkuu wa Wasafi na Msanii nguli Afrika Diamond Platinum akiongea kwenye Usiku wa Mahaba ndi ndi ndi Februari 14, 2022 Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi akiwatambulisha Mawaziri wanaosimamia Sanaa na Habari kwenye usiku wa Mahaba ndi ndi ndi Februari 14, 2022 Mwanamuziki Zuchu akitumbuiza katika Usiku wa Mahaba ndi ndi ndi Februari 14, 2022.
Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa leo Februari 14, 2022 ametoa maelekezo mazito kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) yanayolenga kuboresha mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Maelekezo hayo ameyatoa katika mkutano wa Waandishi wa Habari aliofanya katika Ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo Februari 14 baada ya kufanya kikao na Viongozi wa TFF, BMT na watendaji wa Wizara.
Amefafanua kuwa Serikali ipo katika mikakati kabambe ya kuboresha miundombinu ya michezo katika shule 56 nchini ikiwa ni pamoja na kufunga mashine za kisasa za kufuatilia michezo (VAR) kwenye viwanja vitano kwa kuanzia pamoja na kujenga vituo vikubwa vya michezo.
Akitoa maelekezo ya Serikali, Mhe. Mchengerwa amesema BMT likutane na TFF mara moja kujadili namna ya kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa Sheria na taratibu za mchezo huo pendwa nchini ambapo pia amesisitiza kuwa Kamati inayohusika na Waamuzi ijitafakari kwa kuwa hadi sasa kwenye msimu huu wa ligi tayari imeshawaondoa waamuzi 13 kwa makosa ya upendeleo na rushwa.
Pia amesema TFF likutane na waamuzi wote ili kupata uvumbuzi wa changamoto na sintofahamu zinazoendelea kujitokeza katika mchezo huo kinyume na sheria ambapo TAKUKURU washirikishwe wawepo ili waweze kutoa elimu ya rushwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Amefafanua kuwa iwapo Serikali haitaweza kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu, mchezo huo hautakuwa na maendeleo.
Aidha, amesisitiza waamuzi wasio na sifa waondolewe moja kwa moja na kuwaleta wengine wenye sifa na TFF lihakikishe utekelezaji wa sheria na kanuni za vilabu huku BMT iendelee kusimamia utawala bora ili kuwe na ustawi katika michezo.
Pia ameviomba Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu programu mbalimbali za redio na televisheni kuhusu sheria za mpira wa miguu kupitia kwa wakufunzi na waamuzi.
Katika mkutano huo Mhe. Mchengerwa aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake Dkt. Hassan Abbasi, na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya michezo na Kaimu katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT) na Uongozi wa TFF
Comments
Post a Comment